Binti Fatma Yusuf Adli Hassan, mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa sekondari katika Chuo Kikuu cha al Azhar nchini Misri amefanikiwa kuandika Qur’ani kwa mkono wake kwa muda wa miezi mitano akitumia khati za Uthman Taha.

Hayo yameripotiwa na mtandao wa habari wa al Yaum al Sab’i wa Misri na kuongeza kuwa, binti huyo anasoma masomo ya fasihi na alijaaliwa kuhifadhi Qur’ani nzima akiwa na umri wa miaka 15. Baada ya hapo alianza kuandika kwa mkono wake maneno hayo ya Mwenyezi Mungu na ilimchukua miezi mitano kumaliza kazi hiyo muhimu kwa kutumia khati za Uthman Taha.

Binti Fatma ameuambia mtandao huo wa habari kwamba, lengo lililomsukuma kuandika kwa mkono wake Qur’ani Tukufu ni kusaidia kukilinda Kitabu hicho kitakatifu, kutia nguvu fani ya uandikaji wa khati za Kiarabu na kufanya juhudi za kufananisha khati zake na zile za Uthman Taha; lakini muhimu zaidi anasema ni kuweka kumbukumbu ya kwamba ameweza kufanya kazi muhimu inayomridhisha Allah katika maisha yake. Binti huyo Mmisri mzaliwa wa kijiji cha al Hajj Salaam, cha mji wa Fartosh wa mkoa wa Qena wa kusini mwa Misri aidha amesema, anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumpa fakhari ya kupata taufiki ya kuhifadhi na kuandika Qur’ani nzima katika maisha yake kama ambavyo anamshukuru Allah pia kwa kumpa taufiki ya kushiriki kwenye mashindano mbalimbali ya Qur’ani na kushika nafasi nzuri.

(Visited 18 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!