Wilaya ya Detroit ya jimbo la Michigan nchini Marekani imeitambua rasmi Idul Fitr kuwa sikukuu rasmi kwa wanafunzi Waislamu.
Mtandao wa “Chalkbeat” umeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, baada ya mapambano ya muda mrefu ya kupigania kutambuliwa rasmi sikukuu ya Idul Fitr, hatimaye Shirikisho la Walimu wa wilaya ya Detroit huko Michigan Marekani, limekubali kwamba, kuanzia mwaka ujao wa masomo wa 2021-2022, kuwe na siku tatu za mapumziko kwa ajili ya Sikukuu ya Idul Fitr.
Mapambano ya kupigania kutambuliwa rasmi sikukuu hiyo yalianza mwaka 2018 wakati mwanafunzi Muislamu, Mohammad Muntakim alipoanzisha shule ya ufundi kwa kushirikiana na wanafunzi Waislamu wa vyuo vikuu, na kuanzisha kampeni ya kupigania kutambuliwa rasmi sikukuu ya Idul Fitr.
Juhudi hizo ziliungwa mkono na Ali Yahya, mmoja wa viongozi wa jamii ya Waislamu katika eneo hilo ambapo uungaji mkono wake huo uliongeza kasi katika jitihada za kuwaelimisha walimu na wakuu wa wilaya hiyo na hatimaye juhudi hizo zimezaa matunda.
Mwaka jana wilaya ya Detroit huko Michigan Marekani iliendesha programu maalumu ya masomo kwa walimu wa eneo hilo kuhusu maadhimisho ya sikukuu ya Idul Fitr. Wanafunzi nao waliendesha kampeni ya kusambaza video katika mitandao ya kijamii ambazo ziliwaonesha wanafunzi, walimu, wazazi na kundi la mawakilli wakiunga mkono kutambuliwa rasmi sikukuu hiyo muhimu ya Waislamu.
Hadi hivi sasa kati ya sikukuu za Waislamu, ni Idul Fitr tu ndiyo iliyotambuliwa rasmi katika wilaya hiyo.
Detroit ndio mji mkubwa zaidi na wenye wakazi wengi zaidi katika jimbo la Michigan na ni mji wa 20 kwa kuwa na wakazi wengi zaidi nchini Marekani. Mji huo una takriban wakazi laki saba (700,000). Takwimu za mwaka 2017 zinaonesha kuwa Waislamu wanaunda asilimia 3 ya wakazi wa mji huo.