Kitengo cha Kupambana na Misimamo Mikali cha Chuo Kikuu cha al Azhar cha Misri kimeishukuru serikai ya Ubelgiji kwa kuwatimua na kuwafukuza maadui watano wa Uislamu waliokuwa na nia ya kuchoma moto msahafu na kueneza chuki dhidi ya Uislamu mjini Brussels.

Televisheni ya “”Rusia al Yaum” imetangaza habari hiyo na kukinukuu kitengo hicho muhimu cha Chuo Kikuu cha al Azhar kikisema: Tunamshukuru Waziri wa Masuala ya Wahajiri wa Ubelgiji kwa kuzima fitna hiyo kabla haijatokea na kuwafukuza watu hao wenye misimamo mikali ambao walikuwa wanahatarisha utulivu wa umma nchini humo.

Kimesema, hatua za haraka zilizochukuliwa na viongozi wa Ubelgiji ni ishara nzuri ya kukomeshwa hotuba za chuki na kung’oa mizizi ya ugaidi na ukatili. Hatua hiyo bila ya shaka yoyote itasaidia kuheshimiwa hisia za wengine na itikadi na nembo zao za kidini kwa njia ya moja kwa moja katika kukuza utamaduni wa watu wote kuishi pamoja kwa amani na kwa kuheshimiana. Itakumbukwa kuwa, juzi Alkhamisi, Novemba 12, 2020, serikali ya Ubelgiji iliwatimua nchini humo raia watano wa Denmark kutoka genge lenye misimamo mikali la Stram Kurs linaloongozwa na Rasmus Paludan, adui mkubwa wa Uislamu ambaye mara kwa mara amekuwa akivunjia heshima hadharani matukufu ya Waislamu. Wadenmark hao walikuwa na nia ya kuchoma moto Msahafu katika eneo moja la Waislamu wengi huko Brussels, mji mkuu wa Ubelgiji.

(Visited 39 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!