Kongamano la kwanza kabisa la aina yake kuhusu Waislamu wenye asili ya Afrika limeanza mtandaoni kwa matumaini kwamba litaweza kuutangazia ulimwengu kazi kubwa zilizofanywa na Waislamu hao katika kuitumikia dini tukukfu ya Kiislamu.

Shirika la habari la TRT limeripoti habari hiyo na kumnukuu mmoja wa waandaaji wa kongamano hilo, Bi Naima B. Robert akisema kuwa, kongamano hilo lililoanza jana Ijumaa, Oktoba 2, litaendelea hadi tarehe 25 Oktoba, 2020.

Amesema, jamii ya Waislamu wenye asili ya Afrika kwa muda mrefu wamesahauliwa, hivyo wameitisha kongamano hilo la kwanza kabisa la aina yake ili kuwaenzi na kuutangazia ulimwengu kazi kubwa zilizofanywa na Waislamu wenye asili ya Afrika.

Kongamano hilo limeitishwa baada ya kuuawa Wamarekani wenye asili ya Afrika akiwemo Ahmaud Arbery, Breonna Taylor na George Floyd, na kuzuka wimbi la malalamiko na maandamano yaliyobebwa na kaulimbiu ya “Roho za Watu Weusi ni Muhimu.” Maandamano hayo ya kulaani ubaguzi wa rangi na ukatili wanaofanyiwa Wamarekani wenye asili ya Afrika, yameenea ulimwenguni kote. Wazungumzaji katika kongamano hilo lililoanza jana na kupangwa kuendelea hadi hadi Jumapili ya tarehe 25 mwezi huu wa Oktoba, ni watu muhimu kutoka sekta mbalimbali wakiwemo wahadhiri wa vyuo vikuu, waandishi, wanafikra, watu wenye ushawishi mkubwa katika vyombo vya habari, waandishi wa magazeti n.k. Miongoni mwa maudhui kuu zitakazojadiliwa kwenye kongamano hilo ni usalama wa kisaikolojia, ndoa na malezi ya watoto, uzalishaji mali, biashara n.k.

(Visited 16 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!