Baada ya kuongezeka maandamano ya Waislamu na ususiaji wa bidhaa za Ufaransa, hatimaye rais wa nchi hiyo, Emmanuel Macron ameonekana kulegeza kamba kwa kudai kuwa nchi yake haina uadui na Uislamu wala Waislamu.

Rais huyo wa Ufaransa ametoa matamshi hayo kujibu makala ya gazeti la Uingereza la Financial Times na kudai kuwa gazeti hilo limemnukuu vibaya.

Siku ya Jumanne gazeti la Financial Times lilichapisha makala na ikasemwa kwamba matamshi na misimamo ya Emmanuel Macron inasababisha chuki dhidi ya Waislamu wa Ufaransa.

Rais huyo wa Ufaransa jana Jumatano, Novemba 4, 2020 alimwandikia barua mhariri wa gazeti hilo na kudai limemnukuu vibaya. Gazeti hilo limemshutumu Macron kwamba analenga kuwapaka matope na kuwatuhumu Waislamu wa Ufaransa kwa malengo yake binafsi ya kiuchaguzi. Vile vile limemshutumu rais huyo kuwa analenga kuzusha hali ya hofu na wasiwasi nchini Ufaransa kwa manufaa yake binafsi.

Macron amedai kuwa, kamwe hatoruhusu mtu yeyote kusema kwamba Ufaransa au serikali ya nchi hiyo inawabagua na kuwanyanyasa Waislamu nchini humo.

Tayari makala hiyo ya rais wa Ufaransa imeshafutwa katika tovuti ya gazeti la Financial Times.

Kama ilivyowahi kuripotiwa na tovuti hii ya ahramed14.com, Waislamu katika kona zote za dunia wamechachamaa na kusimama kidete kumuhami Nabii wa rehema, Mtume Muhammad SAW mbele ya maadui zake hasa wa nchini Ufaransa.

Macron alinukuliwa akidai kwamba eti kuna ugaidi na ufashisti wa Kiislamu. Madai hayo yamewakasirisha mno Waislamu kote ulimwenguni huku Mufti wa Oman, Sheikh Ahmad bin Hamad al Khalili akitoa mwito wa kususiwa kikamilifu bidhaa za Ufaransa. Viongozi wakuu wa nchi za Waislamu kama Uturuki, Iran, Pakistan na nyinginezo, nao wamechukua msimamo imara wa kukabiliana na chuki dhidi ya Uislamu na Mtume Muhammad SAW. Vyuo Vikuu vya kidini vya Iran na Misri navyo vimechukua msimamo imara wa kupinga uchokozi huo maadui wa Uislamu.

Msimamo huo imara wa Waislamu unaonekana kuzaa matunda, baada ya Rais Emmanuel Macron ambaye huko nyuma aliunga mkono kuvunjiwa heshima Mtume Muhammad SAW, sasa anadai kuwa nchi yake haina chuki na Uislamu wala na Waislamu.

(Visited 16 times, 1 visits today)
One thought on “Maandamano, ususiaji wa Waislamu wampigisha magoti Macron?”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!