Mahakama ya kiidara nchini Sweden imetoa hukumu ya kufuta marufuku ya Hijab iliyokuwa imewekwa kwa wanafunzi Waislamu katika jimbo la Skåne la kusini mwa nchi hiyo.

Shirika la habari la Anadolu limetangaza habari hiyo na kusema kwamba mahakama ya kiidara ya eneo la Malmo la kusini mwa Sweden, Jumanne, tarehe 17 Novemba 2020 imetangaza kwamba, hukumu ya Baraza la Mji wa Skurup ya kupiga marufuku Hijab kwa wanafunzi Waislamu, imefutwa.

Mahakama hiyo imesisitiza kuwa, hukumu ya baraza la mji huo haikuwa sahihi na ilikuwa inapingana na Katiba ya Sweden ya watu kufuata kwa uhuru itikadi wanazopenda za kidini.

Jumatatu, Novemba 16, 2020, mwakilishi wa Idara Mahakama ya Sweden aliwasilisha maombi ya kufutwa marufuku hiyo kwa sababu inakinzana na Katiba.

Mwezi Disemba, 2019, Manispaa ya mji wa Skurup huko kusini mwa Sweden iliwapiga marufuku wanafunzi Waislamu wenye umri wa chini ya miaka 13 kuvaa Hijab katika maeneo ya skuli.

Hukumu hiyo ilipingwa na watu mbalimbali katika mji huo akiwemo mwalimu mkuu wa skuli moja ya mji wa Skurup, Mattias Liedholm ambaye katika hotuba yake moja alisema kuwa, haitambui marufuku hiyo na ataendelea kuruhusu wanafunzi Waislamu kuingia shuleni pake wakiwa wamevaa mavazi ya staha kama inavyofundishwa na dini yao. Ijapokuwa msimamo wa mwalimu mkuu huyo haukuwapendeza baadhi ya watu ambapo mwezi Februari mwaka huu wa 2020 alianza kupokea ujumbe mbalimbali katika mitandao ya kijamii wa kumtishia kumuua, lakini hakubadilisha msimamo wake.

(Visited 21 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!