Shirika moja maarufu la utafiti ambalo limeasisiwa na linaendeshwa huko Ujerumani na mke na mume Waislamu wenye asili ya Uturuki limeshirikiana na shirika la Kimarekani la Pfizer kutengeneza chanjo ya COVID-19 ambayo hivi sasa dunia imeelekeza matumaini yake makubwa kwake.

Mtandao wa About Islam umeripoti habari hiyo na kusema kuwa, mafanikio ya chanjo hiyo yamekuja wakati huu ambapo maambukizo ya kirusi cha corona yameongezeka sana duniani.

Taarifa za kuaminika zinasema kuwa, mashirika mawili, lile la Pfizer la nchini Marekani na la BioNTech la nchini Ujerumaini lililoasisiwa na Waislamu – mtu na mkewe wenye asili ya Uturuki – yamefanikiwa kuzalisha chanjo inayofanya kazi vizuri kwa asilimia 90 na kuleta matumaini ya kudhibitiwa ugonjwa hatari wa COVID-19, duniani.

Shirika la BioNTech liliasisiwa mwaka 2008 katika mji wa Mainz wa jimbo la Rhineland-Palatinate la kusini magharibi mwa Ujerumani. Waasisi wa shirika hilo ni Waislamu, Bw. Ugur Sahin (55) ambaye ndiye mkuu. Anashirikiana na mkewe Bi Ozlem Tureci (53) kuendesha shirika hilo. Kwa mujibu wa gazeti la The Guardian, Waislamu hao wanashirikiana na mtaalamu wa maradhi ya saratani, Christoph Huber katika kazi zao kwenye kampuni hiyo.

Kwa mujibu wa mtandao wa About Islam, mwaka 2001, Waislamu hao walianzisha kampuni ya Ganymed Pharmaceuticals iliyokuwa inajishughulisha na matibabu ya kensa. Mwaka 2016 waliliuza shirika hilo kwa Euro milioni 422.

Mwaka 2008 walianzisha shirika jingine la BioNTech linaloshughulikia pia matibabu ya kensa na kuzalisha dawa za ugonjwa huo.

Tofauti na chanjo za kijadi ambazo zinatumia virusi dhaifu au vilivyokufa kuingiza katika mwili ili kuimarisha kinga za mwili, chanjo za m-RNA zinazozalishwa na shirika la Waislamu hao linatuma code za kijenetiki katika seli za mwili wa mwanadamu na kuzilazimisha kuzalisha protini na hivyo kuufanya mwili wa mwanadamu uimarishe mfumo wake wa kujilinda na maradhi. Ikumbukwe kuwa, masharti ya Shirika la Chakula na Madawa la Marekani (FDA) kwa wazalishaji wa chanjo ni kuhakikisha chanjo zao zinafanya kazi kwa asilimia isiyopungua 50. Kwa kuzingatia viwango hivyo vya shirika la FDA la Marekani, chanjo ya corona iliyozalishwa na Waislamu hao kwa kushirikiana na shirika la Kimarekani la Pfizer, ina nafasi kubwa ya kukubalika, kwani majaribio yake ya awali yameonyesha uwezo wake wa kufanya kazi kwa asilimia 90.

(Visited 61 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!