Wanawake wanne Waislamu wanaochunga vazi la staha la Hijab wameshinda kesi mahakamani mjini New York Marekani. Wanawake hao Waislamu walifungua kesi mahakamani baada ya kulazimishwa kuvua Hijab zao kwa ajili ya kupigwa picha na jeshi la polisi. Mahakama imetoa hukumu kwa maslahi ya Waislamu kiujumla baada ya kusema kuwa, inabidi sheria zibadilishwe na wanawake Waislamu wanaweza kupiga picha za masuala ya polisi wakiwa wamevaa Hijab zao.

Hayo yameripotiwa na televisheni ya CNN ya Marekani ambayo imesema kuwa, idara ya polisi mjini New York sasa inaruhusu wanawake Waislamu wapige picha na mavazi yao ya staha ya Hijab katika masuala yanayohusiana na jeshi hilo.

Mwaka 2018 wanawake wanne Waislamu walifungua mashtaka mahakamani baada ya jeshi la polisi la New York kuwashinikiza kuvua Hijab zao wakati wa kupigwa picha.

Katika mashtaka yao, Waislamu hao walisema kuwa, uhuru wao wa kiraia umekanyagwa kwani maafisa wa polisi wamewalazimisha kuvua Hijab na kukaa kichwa wazi mbele ya wanaume wakati hilo ni haramu kwa mujibu wa mafundisho ya dini yao.

Mmoja wa Waislamu hao anayejulikana kwa jina la Laila Ibrahim anasema, alikamatwa na polisi mwaka 2018 na kulazimishwa kuvua Hijab mbele ya maafisa chungu nzima wanaume wa polisi. Anasema alipinga sana kukashifiwa Hijab yake na kuwaeleza maafisa wa polisi kwamba kwa mujibu wa itikadi yake ya kidini, hawezi kamwe kuvua Hijab.

Bi Laila ameiambia televisheni ya CNN kwamba maafisa wa polisi walimkatalia hata ombi lake la kupewa mkalimani na mtu wa kumfasiria lugha wakidai hakuna haja. Baada ya hapo afisa mmoja mwanamme wa polisi alimvamia na kumvua kwa nguvu kitambaa cha kichwa na kumuweka kwenye chumba kilichojaa wanaume kwa ajili ya kupigwa picha. Anasema alihishi kudhalilishwa sana na kukata tamaa. Anasema, vazi la staha la Hijab ni sehemu ya utambulisho wa mwanamke Muislamu na bila ya Hijab, utambulisho wa mwanamke Muislamu hauwi kamili.

Amesema ana matumaini sheria mpya itawafanya polisi wa New York waheshimu haki za watu wa imani na itikadi tofauti na hawatowaweka tena chini ya mashinikizo.

Pamoja na hayo bado polisi wa New York wanaruhusiwa kumlazimisha mwanamke Muislamu kuvua Hijab yake wakati wanapotilia shaka masuala ya silaha au magendo kwa sharti kwamba upekuzi huo ufanywe na afisa wa kike wa polisi.

Kwa mujibu wa sheria za Marekani, wanawake Waislamu wanaruhusiwa kuvaa Hijab wakati wanapopiga picha kwa ajili ya leseni za udereva au pasi za kusafiria.

(Visited 32 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!