Picha inayomuonesha Mohamed Salah Hamed Mahrous Ghaly maarufu kwa jina la Mohamed Salah, mshambuliaji nguli wa timu ya Liverpool ya Premier League inayotetea hivi sasa taji la ligi hiyo maarufu ya Uingereza, akiwa anasoma Qur’ani tukufu ndani ya ndege wakati timu ya taifa ya Misri ilipokuwa inaelekea Kenya kwa ajili ya kucheza na timu ya taifa ya nchi hiyo, Harambee Stars, imewavutia mamilioni ya watu katika mitandao ya kijamii.

Leo Alkhamisi saa mbili na nusu usiku kwa majira ya Afrika Mashariki, timu mbili za taifa za Kenya na Misri zinachuana kwa ajili ya kufaulu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika.

Sasa hivi nyota ya Mohamed Salah inang’ara sana kiasi kwamba mchezaji huyo Muislamu anayeipenda dini yake anawekwa daraja moja na magalacha wengine wa soka wa hivi sasa, kama Leonel Messi na Christiano Ronaldo.

Mohamed Salah amefanikiwa kuutangaza vizuri Uislamu kiasi kwamba mashabiki kadhaa wa Liverpool hivi karibuni walitangaza hadharani kwamba kama Salah ataifungia timu hiyo mabao mengine machache tu basi watasilimu na kuingia katika dini tukufu ya Kiislamu.

Huko kwao Misri pia, nguli huyo ambaye anajua vizuri kucheza na nyavu za magolkipa wa daraja zote, anapendwa sana kiasi kwamba katika uchaguzi wa hivi karibuni wa Misri, jina la Mohamed Salah liliandikwa na wapiga kura kwa zaidi ya mara milioni moja katika karatasi za kupigia kura.

Miezi ya hivi karibuni Mohamed Salah ameng’ara zaidi. Miongoni mwa tabia zake nzuri za kuvutia ni kusoma dua kabla ya kila mechi na kumsujudia Mwenyezi Mungu kila anapokuwa na furaha na kusoma Qur’ani muda wote. Hayo ni mambo ambayo yanagonga vichwa vya habari hasa katika ulimwengu wa Kiislamu, muda wote. Tab’an Mohamed Salah si nyota pekee Muislamu katika soka. Bali kuna wachezaji wengine wengi nguli na wakubwa wanacheza katika Premier League ya Uingereza na ligi za nchi nyinginezo na wanafanya vizuri sana katika timu zao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!