Milango ya Misikiti 4000 imefunguliwa baada ya kufungwa kwa zaidi ya miezi 9 kutokana na janga la corona.
Televisheni ya France 24 imetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, Kamati ya Kupambana na COVID-19 ya Tajikistan imesema kuwa imechukua uamuzi huo kutokana na kupungua maambukizo ya kirusi cha corona nchini humo.
Televisheni hiyo ya nchini Ufaransa imetangaza pia kuwa, asubuhi ya Jumatatu, Februari 1, 2021, Misikiti 4000 pamoja na taasisi na vituo mbalimbali vya kidini katika kona zote za Tajikistan, vimefunguliwa.
Tajikistan ina watu milioni 9.5 na takriban wote ni Waislamu.
Adhana zimesikika katika miji yote ya nchi hiyo ya Asia ya Kati ukiwemo mji mkuu Dushanbe. Tajikistan ina watu milioni 9.5 na takriban wote ni Waislamu.
Licha ya kufunguliwa Misikiti hiyo, lakini hatua zote za tahadhari za kujikinga na kirusi cha corona zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na kupiga dawa Misikiti na kuhakikisha Waislamu waliomiminika kwenye Misikiti hiyo wanachunga protokali zote za kiafya.
Misikiti imefungwa mara nchini Tajikistan baada ya kuzuka wimbi la ugonjwa wa COVID-19. Kwanza ilifungwa kwa muda wa wiki mbili mwezi Machi 2020 na mara ya pili ilifungwa kwa zaidi ya miezi 9 kuanzia tarehe 18 Aprili, 2020.
Sasa hivi mamia ya Waislamu na wafuasi wa dini nyinginezo wameruhusiwa kwenda kwenye maeneo ya ibada zao.
Rais Emomali Rahmon wa Tajikistan wiki iliyopita aliwatumia wabunge ujumbe wake wa kila mwaka akiwataka wananchi wasiende misikitini bila ya kuvaa barakoa na kuchunga miongozo ya watu wa afya, vinginevyo Serikali italazimika kuifunga tena. Vile vile ametangaza habari ya kudhibitiwa kikamilifu ugonjwa huo nchini mwake akisema: Tunamshukuru Mwenyezi Mungu ugonjwa wa corona umeondoka nchini mwetu tangu mwezi Januari 2021. Yaani leo hii Tajikistan haina tena ugonjwa wa COVID-19.