Serikali ya Uzbekistan imetangaza kuwa kuanzia Ijumaa ya wiki hii ya tarehe 4 Septemba 2020, misikiti ya nchi hiyo itaanza tena kusaliwa Sala za Ijumaa.
Mtandao wa habari wa “Aki Press” umeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, Waislamu watatakiwa kuvaa barakoa kwa lazima waendapo misikitini. Aidha misikiti hiyo itabidi iwe inapigwa dawa mfululizo ili kupunguza kadiri inavyowezekana maambukizo ya kirusi cha corona.
Aidha Waislamu wametakiwa kuchunga masafa yaani kutosali wakiwa wamebanana au kukurubiana sana.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, serikali ya Uzbekistan imekusudia kufungua kumbi za sinema, thieta na viwanja vya kuchezea watoto ifikapo tarehe 5 Septemba 2020 baada ya kujiridhisha kuwa ugonjwa wa COVID-19 umepungua kwa kiasi kikubwa nchini humo. Ikumbukwe kuwa mji wa kale, wa kihistoria na muhimu sana nchini Uzbekistan unajulikana kwa jina la Bukhara na ndio mji wa mwandishi mkubwa wa hadithi anayejulikana kwa jina maarufu la Imam Bukhari.