Nakala ndefu zaidi ya Qur’ani Tukufu iliyoandikwa kwa mkono kwenye kitambaa cha kilomita 3.1 imezinduliwa nchini India.
Toleo la mtandaoni la gazeti la kila siku la The New Indian Express limeripoti kuwa, fundi mmoja wa charahani nchini India anayejulikana kwa jina la Noushad kwa kushirikiana na wanawe wanne, wamepata taufiki ya kuandika kwa mkono nakala ya Qur’ani Tukufu katika majora kadhaa ya vitambaa waliyoyaunganisha katika jora moja lenye urefu wa kilomita 3.1.
Msahafu huo ndio mrefu zaidi kuwahi kuandikwa kwa mkono katika historia.
Kadharsha Moulavi, mtoto wa Sheikh M K Noushad anayeishi katika kijiji cha Eruva karibu na mji Kayamkulam, wilayani Alappuzha, mkoani Kerala, kusini magharibi mwa India anasema, hamu kubwa ya baba yake tangu zamani ilikuwa ni kuandika kwa mkono Qur’ani nzima juu ya kitambaa.
Sheikh Noushad ni mwalimu wa madrasa iitwayo Tharbiyya Madrasa huko Palluruthy, Ernakulam, kusini magharibi mwa India. Mwenyewe anasema alikuwa na hamu ya kuifanya kazi hiyo tukufu muda mrefu nyuma, lakini majukumu na kazi nyingi zilimkosesha fursa. Hata hivyo baada ya kuzuka ugonjwa wa corona au COVID-19, yeye na wanawe wanne wamepata fursa ya kutimiza ndoto hiyo.
Muhammad Shafi, mwana mwingine wa Sheikh Noushad ambaye ni mwalimu anasema, Qur’ani hiyo unaweza kuisoma kiurahisi kuanzia juzuu ya kwanza hadi ya 30 kwa kuyazungusha majora hayo yaliyounganishwa na kuwa jora moja. Kalamu za rangi mbalimbali zimetumika kwenye kuandika msahafu huo. Shafi anasema, kwa anavyojua yeye, huo ndio msahafu mrefu zaidi duniani. Amesema, msahafu huo hivi sasa unahifadhiwa kwenye sanduku moja kubwa.