Mufti Mkuu wa Misri amelaani shambulio la kigaidi lililofanywa dhidi ya watu waliokuwa wanasoma Qur’ani nchini Afghanistan na kuua na kujeruhi Waislamu wengi.

Mtandao wa habari wa al Masry al Youm umeripoti habari hiyo na kumnukuu Sheikh Shawki Allam akilaani vikali shambulizi la kigaidi dhidi ya mahafali ya Qur’ani Tukufu nchini Afghanistan lililopelekea kuuawa Waislamu 15 na kujeruhiwa wengine 20 bila ya hatia wakiwemo watoto wadogo.

Shambulio hilo lililotokea Alkhamisi, Disemba 17, 2020 na lilifanywa kwa mripuko wa bomu lililokuwa limetegwa garini dhidi ya Waislamu waliokuwa katika mahafali ya Qur’ani Tukufu katika mji wa Gilan, mkoani Ghazni, mashariki mwa Afghanistan.

Mufti Allam amesema, kuua watu wasio na hatia, kuteka watu nyara, kuzusha hofu, wizi na kuwatumia watu vibaya kwa sura yoyote ile kumepigwa marukufu na Uislamu na wanaofanya uhalifu huo wana adhabu kali duniani na Akhera.

Aidha amesema, kuna udharura kwa wapenda haki wote kuungana katika kupiga vita vitendo vya kigaidi kwa nguvu zao zote na kuyataka mataifa ya dunia kuchukua hatua zinazotakiwa tena bila ya ubaguzi katika kupambana na ugaidi, misimamo mikali na uenezaji fitna na mizozo.

Mufti Mkuu wa Misri vile vile amesema, kushambulia mahafali za Qur’ani na watoto walioko darasani kunaonesha jinsi yalivyopotoka kifikra magenge na mapote potofu ambayo hayana elimu yoyote ya dini wala hisia zozote za kibinadamu. Aidha Mufti Allam ametoa mkono wa pole kwa serikali, wananchi wa Afghanistan na familia za Waislamu waliouawa na kujeruhiwa katika mahafali hayo ya Qur’ani Tukufu na kuwaombea maghufira kwa Mwenyezi Mungu na afueni ya haraka.

(Visited 14 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!