Serikali ya Pakistan imeamua kuanzisha kituo maalumu cha kuangalia mwezi mwandamo kisayansi na kiteknolojia, wakati huu wa kukaribia kuingia mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Mtandao wa habari wa The Nation umeripoti kuwa, kituo hicho kitafunguliwa rasmi tarehe 12 mwezi huu wa Aprili, 2021 na Waziri wa Sayansi na Teknolojia wa Pakistan, Fawad Chaudhry. Lengo la kuanzishwa kituo hicho ni kupima mzunguko wa mwezi, kujua kiutaalamu vituo vyake, kuzaliwa kwake na wakati wa mwezi mwandamo wakati wa kuchomoza hilal na kuonekana kwa macho.
Kituo hicho kimejengwa karibu na Makumbusho ya Pakistan, pembeni mwa Bustani ya Taifa ya Shakar Parian, mjini Islamabad. Kituo hicho kitaisaidia sana kalenda ya Kiislamu kwani kitakuwa kinaangalia kwa kina na kwa njia sahihi mwandamo wa mwezi katika miezi yote 12 ya mwaka.
Sambamba na kuanzisha kituo hicho, Wizara ya Sayansi na Teknolojia ya Pakistan imeanzisha pia aplikesheni ya Android ijulikanayo kwa jina la “The Ruet” kwa ajili ya kutoa taarifa za miandamo ya mwezi za kituo hicho.
Kwa mujibu wa mtandao wa The Nation wa Pakistan, katika kipindi kifupi tu cha tangu kuanzishwa aplikesheni ya “The Ruet” makumi ya maelfu ya watu wameipakia na kuingiza kwenye vifaa vyao aplikesheni hiyo, suala ambalo linaonesha jinsi watu walivyo na kiu ya kupata taarifa sahihi kuhusu miandamo ya mwezi. Katika mazungumzo yake na Mkuu wa Kamati ya Kuangalia Mwezi Mwandamo ya Pakistan, Maulana Abdul Khabir Azad, Waziri wa Sayansi na Teknolojia wa Pakistan ameitaka kamati hiyo ifanye juhudi zake zote kuhakikisha kuwa inatoa taarifa sahihi na za kuaminika za mwandamo mwezi wa Ramadhani na sikukuu ya Idul Fitr ya mwaka huu.