Jumba la Makumbusho ya Ustaarabu wa Kiislamu la Sharjah nchini Imarati (UAE) ni moja ya makumbusho makubwa zaidi katika ukanda mzima wa magharibi mwa Asia. Miongoni mwa vitu vya thamani na vya kale vinavyohifadhiwa katika makumbusho hayo, ni maandishi nadra na ya zamani sana ya Qur’ani Tukufu.
Makumbusho hayo yalifunguliwa rasmi mwaka 2008. Katika Makumbusho hayo kuna turathi nyingi za ustaarabu na utamaduni wa Kiislamu zinazokadiriwa kufikia 5000.
Miongoni mwa turathi hizo ni nguo za kale za kivita, vifaa vya khat au kaligrafia (Calligraphy), uhunzi na uchongaji, sanaa ya seramiki, sarafu za kale, mawe ya thamani, nakala za kaligrafia, feleji na vifaa vya kielimu na kisayansi.
Huko nyuma Makumbusho hayo yalijulikana kwa jina la Makumbusho ya Kiislamu na yalifunguliwa mwaka 1996 kabla ya kuhamishiwa katika jengo jipya la hivi sasa. Makumbusho hayo yana maeneo saba ya maonesho. Sehemu moja ya maeneo hayo ni maalumu kwa ajili ya nakala za Misahafu ya kale kabisa ya Qur’ani Tukufu.