Kamishna Mkuu wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa amewasilisha ripoti yake na kusema kuwa, mashambulizi na unyama unaofanywa na jeshi na mabudha dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya na raia wa kawaida huko Mynamar (Burma) ambao ulianza mwaka 2017, bado unaendelea. Amesema baadhi ya vitendo hivyo ni jinai za kivita na ni jinai dhidi ya ubinadamu.

Shirika la habari la Anadolu limemnukuu Bi Michelle Bachelet, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa akisema hayo katika ripoti yake hiyo na kuongeza kuwa, Waislamu wa eneo la Arakan huko Myanmar na watu wa kaumu na jamii nyinginezo wangali wanakandamizwa na kufanyiwa ukatili na jeshi na mabudha. Baadhi ya raia wa kawaida wanatoweka bila ya kujulikana waliko na haki zao zinakanyagwa vibaya. Miongoni mwa ukatili wanaofanyiwa ni kuuliwa kiholela, kufukuzwa kwenye maeneo yao kwa umati, kuchomewa moto nyumba na mashamba yao, kutekwa na kuwekwa kizuizini kiholela, kuteswa, vifo vya kutatanisha katika korokoro na kuharibiwa mali zao.

Waislamu wa Myanmar (Burma) wakilia kwa uchungu katika dua

Bi Bachelet amesema, baadhi ya raia wanashambuliwa bila sababu huko Myanmar na ametahadharisha kuhusu kutokea jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu nchini humo.

Amesema, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa pamoja na Baraza la Haki za Binadamu la umoja huo linaitaka serikali ya Myanmar itoe majibu kuhusu jinai hizo. Amesema, inasikitisha kuona kuwa serikali hiyo haichukui hatua yoyote ya kuwalinda Waislamu na watu wengine wa jamii za wachache. Wiki mbili zilizopita pia, wanajeshi wawili wa Myanmar walikiri kwamba walishiriki katika mauaji na ukatili dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya na baadaye kuwazika kwenye makaburi ya umati pamoja na kuwanajisi wanawake wa jamii hiyo.

(Visited 59 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!