Kundi moja la Waislamu na Wakristo nchini Ufilipino wameamua kushirikiana kusafisha mazingira kwa kuanzia kusafisha fukwe za baharini kwa pamoja.
Hayo yameripotiwa na mtandao wa habari wa “UCANews” na kuongeza kuwa, kundi la Waislamu na Wakristo wa Ufilipino jana Alkhamisi Septemba 3, 2020 walifanya kazi kwa pamoja ya kusafisha fukwe za kisiwa cha Palawan zilizokuwa zimejaa takataka.
Kwa upande wake, Alhajj Arturo Suizo, kiongozi wa Waislamu wa eneo hilo walioshiriki kwenye kampeni hiyo amesema kuwa, dini tukufu ya Kiislamu inalipa umuhimu mkubwa suala la kulinda mazingira.
Amesema, Mwenyezi Mungu ametuumba sisi wanadamu ili tulinde mazingira yake. Mazingira ya ulimwengu si mali yetu, bali Allah ametukabidhi tu tuyatumie na tuyatunze.
Alhajj Arturo Suizo ameongeza kuwa, sayari ya ardhi inapaswa kuwa kijani na nzuri na Mwenyezi Mungu ametuumba wanadamu tuwe walinzi wa mazingira na hayo ndiyo mafundisho ya Mtume Muhammad SAW.
Vile vile amewashukuru Wakristo waliojitokeza kushiriki katika jambo hilo la kheri na kusema kuwa, kwa ushirikiano wao huo, wananchi wa Ufilipino wamewaonesha walimwengu kuwa wanaweza kuishi kwa kuvumiliana.
Kisiwa cha Palawan huko Ufilipino ni miongoni mwa vituo vikuu vya utalii kutokana na fukwe zake za mchanga mweupe, misitu ya kijani kibichi na wanyamapori.
Mwaka 2017 kisiwa hicho kilitajwa na jarida moja maarufu la masuala ya utalii kwamba ndicho kisiwa chenye mazingira ya kuvutia zaidi duniani.
Dini tukufu ya Kiislamu inawahimiza sana wanadamu kutembea katika maeneo mbalimbali ya ardhi kuona uwezo wa Mwenyezi Mungu. Utalii unaochunga mafundisho ya Uislamu haukatazwi katika dini hii tukufu ya Mwenyezi Mungu.

(Visited 46 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!