“Mapambano na Mafanikio ya Waislamu wenye asili ya Afrika” imeteuliwa kuwa kaulimbiu ya ratiba maalumu za “Mwezi wa Historia ya Waislamu” ambao huadhimishwa kila mwaka nchini Canada.
Mtandao wa “Muslim Link” umeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, mwezi Oktoba kila mwaka, unatambuliwa nchini Canada kuwa ni “Mwezi wa Historia ya Waislamu.” Ndani ya mwezi huo huwa kunafanyika sherehe, mikutano, makongamano na maonyesho mbalimbali katika kona zote za Canada kwa ajili ya kuwaelewesha watu wa nchi hiyo ya Amerika Kaskazini, utamaduni, itikadi na historia ya Uislamu.
Kaulimbiu ya mwaka huu ya sherehe hizo ni “Mapambano na Mafanikio ya Waislamu wenye Asili ya Afrika” na lengo lake ni kuwatangaza Waislamu mashuhuri wenye asili ya bara la Afrika na kuonyesha mapambano na mafanikio yao.
Katika bango la sherehe za mwaka huu kunaonekana picha za watu mashuhuri kama vile Ayuba Suleiman Diallo, mwanamapambano Muislamu wa karne ya 18 ambaye alisimama imara kupambana na biashara ya utumwa katika bara la Amerika wakati wa ukoloni. Katika bango hilo anaonekana pia mwanamasumbwi bingwa, Muhammed Ali pamoja na mwanamapambano maarufu wa Marekani, Malcom X.
Mwaka 1734 Thomas Bluett aliandika katika kitabu chake kumbukumbu za mwanamapambano Muislamu na Mwafrika, Ayuba Suleiman Diallo. Kitabu hicho ni katika marejeo nadra sana kuhusu mapambano ya karne ya 18 dhidi ya utumwa. Mwaka huu, Rudolph Ware, mhadhiri wa chuo kikuu wa masuala ya historia ameandaa ratiba maalumu katika Shule za Msingi za Canada kwa ajili ya kuwatambulia wanafunzi wa skuli za nchi hiyo; historia na utamaduni wa Waislamu Waafrika nchini Canada.