Wanawake 66 wamefanikiwa kuingia katika fainali za mashindano ya kitaifa ya kuhifadhi Qur’ani Tukufu nchini Iraq, mashindano ambayo yanaendeshwa na kusimamiwa kikamilifu na wanawake wenyewe.
Tovuti ya “Markaz al Qur’an al Karim” wa nchini Iraq umeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, fainali hizo zilianza Jumatano tarehe 4 Agosti na zinamalizika leo Ijumaa tarehe 6 Agosti 2021. Fainali hizo zinafanyika kwa njia ya Intaneti kutokana na sheria kali za kujikinga na maambukizo ya ugonjwa wa corona.
Bi Dalal Tabatabai, mmoja wa waendeshaji wa fainali hizo amesema kuwa, wanawake 193 walichuana katika mashindano ya daraja tatu za hifdh ya Qur’ani nzima, hifdh ya juzuu 20 na hifdh ya juzuu 10 na mwishowe wanawake 66 wamefanikiwa kuingia kwenye fainali hizo.
Amesema, mashindano ya mchujo yalifanyika kwa mawasiliano mubashara ya Intaneti baina ya majaji na washiriki, na hatimaye kwa kutegemea vigezo mbalimbali vilivyozingatiwa na majaji, wanawake 66 wameingia kwenye fainali. Ametoa ufafanuzi zaidi kwa kusema kuwa, majaji wote ni wanawake waliobobea katika fani za Qur’ani Tukufu zikiwemo hifdh nzuri, hukumu za usomaji, sauti, lahani na naghma, kuchunga vituo na uanzaji wa usomaji wa Qur’ani na mbinu zote zinazohusiana na fani hiyo.