Msikiti mkuu wa al Aqsa huko Berlin, mji mkuu wa Ujerumani, Alkhamisi, Novemba 12, 2020 ulivamiwa na watu wasiojulikana.
Mtandao wa habari wa “al Umma” umeripoti habari hiyo na kumnukuu mkuu wa jumuiya ya msikiti huo “Shinasi Yashar (?)” (شیناسی یاشار) akisema kwamba, Alkhamisi asubuhi, msimamiaji wa msikiti huo unaomilikiwa na Umoja wa Kiislamu wa Waturuki wa Ujerumani (DITIB) waliona maandishi ya matusi na kejeli dhidi ya Waislamu katika ukuta wa nyuma ya msikiti huo na katika vioo vya sehemu moja ya kujisaidia.
Amesema, baada ya kuona hali hiyo waliwajulisha polisi ambao walifikia eneo la uhalifu huo na kuanza kufanya uchunguzi.
Huku hayo yakiripotiwa, shirika la habari la Reuters, limewanukuu maafisa wa mji wa Berlin wakisema leo Ijumaa, Novemba 13, 2020, kwamba waendesha mashtaka mjini humo wamewafikisha kizimbani watu 12 kwa kupanga njama za kushambulia misikiti na kuua na kujeruhi Waislamu wengi kadiri inavyowezekana.
Waendesha mashtaka hao wamesema katika taarifa iliyonukuliwa na Reuters kwamba watu hao walikuwa na mpango wa kushambulia misikiti na kuua na kujeruhi idadi kubwa ya Waislamu kadiri inavyowezekana na kuzusha hali ya vita vya ndani nchini Ujerumani.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, maadui hao wa Uislamu walikusanya fedha nyingi, zipatazo euro 50,000 ($59,000) kwa ajili ya kununua silaha. Taarifa hiyo aidha imesema, genge hilo ni la watu 12 na wote ni Wajerumani. 11 kati yao wameshatiwa mbaroni na mmoja bado anasakwa.