Sherehe za kuzindua makumbusho ya Waislamu 51 waliouawa shahidi misikitini huko New Zealand zimeongozwa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Bi Jacinda Ardern.
Vyombo mbalimbali vya habari vimeripoti kwa wingi habari hiyo na kuongeza kuwa Bi Jacinda Ardern ambaye pia ni mkuu wa chama cha Leba cha nchi hiyo, ameshiriki kwenye sherehe za uzinduzi huo akiwa mgeni rasmi. Kwa heshima ya Waislamu Bi Jacinda Ardern ameamua kuvaa mavazi ya staha ikiwa ni pamoja na mtandio kichwani na kuelezea kusikitishwa sana na jinai waliyofanyiwa Waislamu wa nchi hiyo na gaidi mmoja mbaguzi wa rangi mwenye chuki za kidini.
Bi Jacinda Ardern ameahidi kwamba serikali ya New Zealand itaweka sheria kali zaidi za kupiga marufuku matangazo ya ubaguzi wa rangi, ya kueneza chuki dhidi ya Waislamu na ya kuchochea machafuko na uhasama baina ya watu wa dini tofauti.
Itakumbukwa kuwa, gaidi Brenton Tarrant, raia wa Australia ambaye alikiri mahakamani kuwa na imani ya kujiona bora kama mzungu dhidi ya watu wengine, aliwaua kwa umati kuwapiga risasi Waislamu 51 waliokuwa wanasali katika misikiti miwili ya mji wa Christchurch tarehe 15, Machi 2019.
Mwishoni mwa mwezi Agosti 2020 gaidi huyo alihukumiwa kifungo cha maisha jela huko New Zealand. Hapa chini tumeweka baadhi ya picha za uzinduzi wa kumbukumbu za Waislamu hao zilizoongozwa na Waziri Mkuu wa New Zealand, Bi Jacinda Ardern.