- Allah jina takatifu, naanza ya Rahmani
Kwa jina Lako Latwifu, baraka za Ramadhani
Samehe hai na wafu, sote tuwe neemani
Rabi turuzuku toba, ni kumi la ghufurani.
***
- Turudi Kwake Raufu, Yaayyuha waumini
Tusijifanye vipofu, kuasi wetu Manani
Tujipange safusafu, kwa toba misikitini
Rabbi turuzuku toba, ni kumi la ghufurani.
***
- Allah Rabbi utuafu, tumezama madhambini
Mja kiumbe dhaifu, hajali jema ni nini
Hutesa hata siafu, amshinda hayawani
Rabbi turuzuku toba, ni kumi la ghufurani.
***
- Nyoyo zetu zi jafafu, ni kavu hatubaini
Rutubaye ni hafifu, tarutubishwa na nini
Kama si zako Arifu, kwa wajao samahani
Rabi turuzuku toba, ni kumi la ghufurani.
***
- Tutende uadilifu, amri ya yetu dini
Tusione takilifu, kurejea kwa Rabbani
Nyoyo ziingie khofu, tujue tu masikini
Rabi turuzuku toba, ni kumi la ghufurani.
***
- Mola wetu ni Latifu, twaasi tu madhambini
Atusamehe Raufu, huruma nyingi pomoni
Kumi hili takatifu, fursa tusitupeni
Rabi turuzuku toba, ni kumi la ghufurani.
***
- Leo hai kesho mfu, zitajapita awani
Bila ya Mola kukhofu, hakuna cha nusurani
Toba kitu maalufu, tutubu dhambi jamani
Rabi turuzuku toba, ni kumi la ghufurani.
Na Ahmed Rashid.