Sheikh Mkuu wa Chuo Kikuu cha kidini cha al Azhar cha Misri ambaye ni maarufu kwa jina la Sheikh al Azhar, amekosoa vikali uenezaji wa istilahi pandikizi ya “Dini za Ibrahim” akionya kwamba, njama za kuziunganisha pamoja dini tatu za Kiyahudi, Kikristo na Kiislamu kwa madai ya “Dini za Ibrahim” kwa kisingizio cha kuleta umoja wa kidini, kunapingana na haki ya kila mtu ya kufuata itikadi anayotaka, na ni kinyume cha mafundisho ya Uislamu.

Gazeti la “al Rai al Yaum” limemnukuu Sheikh Ahmad al Tayyib akisema hayo Jumatatu kwenye mkutano na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha al Azhar na kusisitiza kukwa, istilahi hiyo sawa kabisa na istilahi nyinginezo kama utandawazi, zinalenga kusambaratisha itikadi za kidini na matukufu ya kimaadili duniani.

Sheikh al Azhar ameongeza kuwa, ijapokuwa kijuujuu inaonekana suala la kulingania umoja katika jamii ya mwanadamu ni jambo zuri, hasa kwa vile umoja na mshikamano huondoa sababu za mapigano na ugomvi, lakini lengo la njama hizi mpya za kuunganisha dini za Uislamu, Uyahudi na Ukristo kwa madai ya “Dini za Ibrahim,” kunalenga kuangamiza matukufu ya kibinadamu yaani uhuru wa kuamini na kufuata mtu itikadi anayotaka. 

Sheikh Mkuu wa Chuo Kikuu cha kidini cha al Azhar cha Misri, Sheikh Ahmad al Tayyib

Amesema, ninavyoamini mimi ni kwamba haiwezekani kuwakusanya watu wote katika dini moja na kuweza watu hao kubakia katika itikadi hiyo hiyo moja. Mwenyezi Mungu ameumba tofauti katika kila kitu, kukanzia rangi na itikadi hadi uwezo wa kufikiri, lugha na asili zake, bali hata alama za vidole na macho ya wanadamu ni tofauti. Yote hayo ni uhakika wa kihistoria na kielimu na muhimu zaidi kuliko yote, huo ni uhakika uliobainishwa ndani ya Qur’ani Tukufu kwamba Mwenyezi Mungu amewaumba watu katika mataifa na rangi tofauti. Iwapo Mwenyezi Mungu angelitaka angeliwaumba watu wote katika itikadi moja, rangi moja, lugha moja na welewa mmoja, lakini Mwenyewe Muumba hakupanga hivyo. 

Ikumbukwe kuwa hivi sasa kumekuwa kukienezwa sana istilahi pandikizi ya “Dini za Ibrahim” na inadaiwa kuwa lengo lake ni kuwa na dini moja inayojumuisha pamoja dini tatu za Uislamu, Uyahudi na Ukristo kwa ajili ya kukabiliana na changamoto na vita baina ya wanadamu. Istilahi hiyo imepata nguvu zaidi baada ya baadhi ya nchi za Kiarabu kutangaza uhusiano wa kawaida na Israel.

(Visited 15 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!