Baada ya kundi moja la Mayahudi kuuvunjia heshima Msikiti wa Nabii Musa AS huko Palestina, makumi ya Wapalestina wamemiminika kwenye Msikiti huo na kusali Sala ya jamaa, ili kuonesha uungaji mkono wao kwa nyumba hiyo ya Allah na kukasirishwa kwao na jinai ya Mayahudi hao wenye misimamo mikali.

Hayo yameripotiwa na shirika la habari la Quds ambalo limeongeza kuwa, baada ya kuenea video katika mitandao ya kijamii zinazoonesha Mayahudi wakiwa ndani ya Msikiti wa Nabii Musa AS katika mji mtakatifu wa Baytul Muqaddas huko Palestina wakiwa wanakunywa pombe, wanapiga muziki, wanaimba nyimbo na kupiga vigelegele, vifijo na kucheza muziki, Waislamu wa Palestina wamekasirika mno na kumiminika haraka kwenye Msikiti huo mtukufu wa kihistoria. Mbali na kusoma Adhana, makumi ya Waislamu hao wa Palestina wamesali pia Sala ya Laasiri kwa jamaa na kulaani vikali jinai ya kundi hilo la Mayahudi lenye misimamo ya kufurutu mipaka.

Waislamu wa Palestina wakisali Sala ya Laasiri katika Msikiti wa Nabii Musa AS baada ya Mayahudi kuuvunjia heshima

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wakati vijana wa Palestina walipoingia ndani ya Msikiti huo, walitangaza kwa sauti kubwa kwamba: “Taifa ambalo kiongozi wake ni Muhammad SAW, kamwe haliwezi kusalimu amri.”

Habari nyingine inasema kuwa, Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Mohammad Shtayyeh ametaka kuundwe kamati maalumu ya kufuatilia kitendo hicho cha kihalifu kilichofanywa na Mayahudi hao katika eneo hilo takatifu la Waislamu. Kwa upande wake, Sabri Saidam, mmoja wa viongozi wa harakati ya HAMAS amesema: Hatukubaliani na kitendo cha mtu yeyote asiye Muislamu au Mpalestina kuingia katika eneo hilo, na tunasubiri kwa shauku kubwa ripoti ya kamati ya kufuatilia uhalifu huo. Harakati ya Jihad al Islami ya Palestina nayo pia imetoa tamko na kusema kuwa, kitendo cha Mayahudi hao cha kufanya sherehe, kupiga mayowe, nderemo na vifijo, kunywa pombe na kupiga na kucheza muziki ndani ya eneo hilo takatifu ni uvunjaji wa wazi kabisa wa heshima ya Msikiti huo. Taarifa ya harakati hiyo aidha imesema, huo si ubinadamu, si utamaduni, si maadili na si jambo linalokubaliwa na dini yoyote ile, hivyo tunalilaani vikali.

(Visited 1 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!