Bunge la Ufilipino limepasisha tarehe Mosi Febrauri kuwa Siku ya Taifa ya Hijab kama ambavyo bunge hilo limetambua rasmi pia uwepo wa Baraza la Taifa la Waislamu wa Ufilipino likiwa ni chombo kikuu cha kusimamia masuala ya Waislalmu na kuongeza welewa na elimu kuhusu vazi la staha la Hijab.

Vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo televisheni ya CNN ya Marekani na shirika la habari la MINA vimetangaza habari hiyo na kusema kuwa, tarehe Mosi Februari kila mwaka imetengezwa nchini Ufilipino kuwa Siku ya Taifa ya Hijab ili kutoa fursa ya kuelimishwa zaidi watu kuhusu vazi hilo la staha ya mwanamke wa Kiislamu.

Wabunge 274 wa Ufilipino wameupigia kura ya ndio muswada nambari 5693 na kuipasisha rasmi tarehe Mosi Februari kuwa siku ya taifa ya vazi hilo tukufu la Waislamu.

Wabunge walioupigia kura ya ndio muswada huo wamesema kuwa, lengo lao ni kuwahamasisha wanawake kujisitiri vizuri na kuvaa vazi la staha la Hijab, kukomesha ubaguzi dhidi ya watu ambao wanachunga ustaarabu huo na kuondoa fikra potofu kuhusu vazi hilo tukufu.

Muswada huo umesema, siku ya kwanza ya mwezi wa Februari ni siku ya kulinda haki za wanawake wanaovaa Hijab na wanaochunga mafundisho ya Uislamu. Inabidi fursa hiyo itumiwe kuwashajiisha wanawake Waislamu na wasio Waislamu kuvaa vazi hilo la staha.

Ikumbukwe kuwa, Siku ya Kimataifa ya Hijab huadhimishwa pia tarehe Mosi Februari kila mwaka katika nchi 276 duniani. Siku hiyo ni katika ubunifu wa Bi Nazma Khan, mwanamke wa Kiislamu raia wa Marekani ambaye alikuja na ubunifu huo baada ya kuongezeka chuki dhidi ya Uislamu kufuatia mashambulio ya tarehe 11 Septemba nchini Marekani. Siku ya Kimataifa ya Hijab ni maarufu hata kati ya wanawake wasio Waislamu huko Marekani na katika nchi mbalimbali duniani.

Baadhi ya wanawake wasio Waislamu huvaa Hijab siku hiyo na kuweka picha zao katika mitandao ya kijamii kama vile Facebook.

(Visited 16 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!