Taasisi ya Masuala ya Kidini ya Uturuki imetangaza kuwa itagawa nakala  90,000 za Qur’ani Tukufu katika nchi 36 tofauti za dunia wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani wa mwaka huu wa 1442 Hijria.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Anadolu la Uturuki, Ihsan Acik, Naibu wa Mkuu wa Bodi ya Taasisi ya Masuala ya Kidini ya Uturuki amesema Jumapili, Aprili 11, 2021 kwamba taasisi hiyo imekusudia kugawa nakala 90 elfu za Qur’ani Tukufu katika nchi 36 duniani wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani unaotarajiwa kuanza wiki hii katika kona mbalimbali za dunia.

Amesema, tuna nia ya kutoa misaada ya kifedha na kiroho kwa wanyonge na wanaodhulumiwa katika kona mbalimbali za dunia wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Aidha amesema, miongoni mwa ratiba za taasisi hiyo wakati wa Ramadhani itakuwa ni kuwapa watu futari, nguo, zaka na mambo yote yatakayowasaidia Waislamu kufunga vizuri na kusherehekea kwa furaha sikukuu ya Idul Fitr.

Amesema zoezi hilo wamekuwa wakilifanya tangu mwaka 2015 kwa shabaha ya kuwafikishia walimwengu ujumbe mtukufu wa Qur’ani Tukufu katika kona zote za dunia. Mwaka jana, Taasisi ya Masuala ya Kidini ya Uturuki ilitangaza kuwa, tangu mwaka 2015 hadi hivi sasa imegawa karibu nakala milioni moja katika nchi zipatazo 90 tofauti ulimwenguni.

(Visited 40 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!